Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo, Chadema kimesema kwamba kilifikia uamuzi wa kumvua nyadhifa zake, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wake, Zitto Kabwe kutokana na sababu moja tu ya kuhusika katika Waraka wa Mkakati wa Mabadiliko 2013.
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu
aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kwamba waraka huo
unaeleza mbinu za uasi ambazo zililenga kufanya mabadiliko makubwa ya
kiuongozi wakati wa uchaguzi mkuu wa ndani wa chama hicho jambo ambalo
ni kinyume na katiba, sheria na itifaki za Chadema.
Hivi karibuni, Kamati Kuu ya Chadema iliwavua
nyadhifa zao, Zitto, Mjumbe wa Kamati Kuu, Dk Kitila Mkumbo na
Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Samson Mwigamba kutokana na madai hayo.
Siku tatu zilizopita, Zitto na Dk Kitila
waliitisha mkutano wa wanahabari na kueleza sababu mbalimbali za
kung’olewa kwao ikiwamo suala la posho na ruzuku za vyama vya siasa.
“Wamefukuzwa katika uongozi kutokana na kuandaa
mpango wa mapinduzi uliopo katika waraka wa ‘Mkakati wa Mabadiliko
2013,” alisema Lissu na kuongeza:
“Hawa wote hawakuvuliwa madaraka kwa sababu ya
taarifa za Kamati ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), kuhusu ukaguzi
wa hesabu za chama, suala la posho kwa wabunge wala kuuza majimbo ya
uchaguzi mwaka 2010.”
Alisema kutokana na kosa hilo, Sekretarieti ya
Kamati Kuu ya Chadema ilikutana juzi kupitia uamuzi wa kikao cha Kamati
Kuu na kuridhika nao, “Leo (jana) wahusika wote watapatiwa barua zao
zilizoorodhesha makosa yao kumi na moja wanayotakiwa kujibu ndani ya
siku 14.” Bila ya kuyataja, Lissu alisema makosa hayo yote yamejikita
katika waraka huo.
Mnyika pia alijibu hoja zilizotolewa na Wakili wa
kujitegemea na Diwani wa Kata ya Mabogini mkoani Kilimanjaro (Chadema),
Albert Msando juu ya kasoro wakati wa kutoa hukumu kwa makosa ya Zitto
na Dk Kitila, ikiwa ni pamoja na kukiukwa kwa katiba ya chama
inayoeleza kuwa mtu hatachukuliwa hatua za kinidhamu kabla ya kupewa
mashtaka kwa maandishi na mamlaka husika na kupewa nafasi ya kuyajibu
kwa maandishi.
Mnyika alisema, “Zitto na Dk Kitila hawakumwambia
wakili wao ukweli kwamba kanuni hii ya chama ilishafanyiwa marekebisho
muda mrefu na Baraza Kuu la chama na kuongezwa kifungu (d), ambacho
kinasema: “Kamati Kuu inaweza kuchukua hatua za dharura kama inaona
masilahi ya chama yanaathiriwa.”
Waraka
Mnyika alisema waraka uliowang’oa Zitto na Dk
Kitila ambao umechapishwa katika magazeti mbalimbali pamoja na mitandao
ya kijamii, siyo ule uliowasilishwa katika Kikao cha Kamati Kuu.
“Waraka utakaotumika katika mashtaka yao siyo huo.
Sisi tutautumia ule ambao uliwasilishwa katika Kamati Kuu ambao una
mambo makubwa na mengi zaidi kuliko huo unaochapishwa sehemu mbalimbali,
ikibidi tutautoa huo waraka halisi,” alisema.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Zingatia: Mwanachama wa blogu hii tu ndiye anayeweza kuchapisha maoni.